TAG Southern Bible College P.O. Box 165, Mbeya (+255)715-865-880 [email protected]

Historia ya Chuo cha TAG Southern Bible College

Historia ya TAG SBC

Chuo cha Biblia Mbeya ambacho kwa sasa kinaitwa Southern Bible College ndicho chuo cha kwanza kuanzishwa katika kanisa la Tanzania Assemblies of God. Kilianzishwa na Mmishenari Wesley Hurst mwaka 1954.

Free Bootstrap Template by uicookes.com

SBC ni Chuo cha Tanzania Assemblies of God

Chuo cha Biblia Mbeya ambacho kwa sasa kinaitwa Southern Bible College ndicho chuo cha kwanza kuanzishwa katika kanisa la Tanzania Assemblies of God. Kilianzishwa na Mmishenari Wesley Hurst mwaka 1954.

Mmishenari Hurst alifika Mbeya tarehe 14/6/1952 akitokea Marekani ili kusaidia kazi ya kuendeleza uamsho mkubwa ambao ulikuwa umepamba moto kule kusini mwa Tanzania

Mmishenari Hurst alitumwa toka makao makuu ya Assemblies of God Marekani baada ya Mmishenari Ragner Udd kuomba aletwe mmishenari wa kumsaidia huduma ya kuandaa watumishi. Wamishenari Udd na Hurst wakisaidiana na Mchungaji Moses Kameta, walitafuta eneo la ardhi kwa ajili ya kujenga Chuo. Walifanikiwa kupata eneo lenye ukubwa wa ekari 20, ambalo walipewa na kiongozi wa kimila wa kabila la Wasafwa, Chifu Mwalyego wa Utengule. Eneo hilo lipo katika Kata ya Kalobe karibu na kijiji cha Itende, kilometa mbili na nusu kutoka barabara kuu iendayo Tunduma. Sehemu kubwa ya ardhi hiyo ilitaifishwa na serikali baada ya Azimio la Arusha na kubaki ekari saba na nusu.

Mmishenari Wesley Hurst alianza kutekeleza maono ya kuwa na Chuo cha Biblia mnamo 1952 kwa kusimika mahema ambayo yalitumika kama madarasa ya shule ya msingi na ya mafunzo ya elimu ya Biblia kwa wachungaji. Mwaka 1953 alianza kujenga mabweni kwa ajili ya Chuo cha Biblia. Baada ya kumaliza ujenzi wa mabweni mwaka 1954, Chuo kilifunguliwa rasmi na Mmishenari Hurst akawa Mkuu wa Chuo wa kwanza

Walimu wa kwanza katika chuo hicho walikuwa ni Wamishenari na wake zao. Mchungaji Moses Kameta aliwasaidia kutafsiri, kwa sababu lugha iliyotumika kufundishia ilikuwa ni Kinyakyusa. Kusudi la chuo hiki lilikuwa ni kuwaandaa watumishi wazawa wa Tanganyika kwa ajili ya huduma. Chuo kilipoanza kilijulikana kwa jina la Maranatha Bible College jina hilo lilibadilshwa na kuwa Tanganyika Bible Institute. Baadaye chuo kilibadilishwa jina kikaitwa International Bible College; kisha tena kikaitwa Mbeya Bible College na sasa kinajulikana kama Southern Bible College.

Chuo cha Mbeya kina mchango mkubwa sana katika kukua kwa Kanisa la Tanzania Assemblies of God. Miongoni mwa wanafunzi wa kwanza waliosajiliwa kusoma ni Mchungaji Yohana Mpayo, Mchungaji Ramsey Mwambipile, Mchungaji David Mwainyekule na Mchungaji Asajigwe Mwaisabila. Wachungaji hao walikuwa kichocheo kikubwa kwa uamsho wa kwanza katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God.

Pamoja na mchango wake katika kuendeleza elimu kwa njia ya kuanzisha Chuo cha Biblia, Mmishenari Hurst pia alichangia kwa kufanya yafuatayo: Aliandaa mpango mzuri wa kutunza na kutumia sadaka na mafungu ya kumi; Alianzisha shule ya Jumapili (Shule ya Uanafunzi); Alisimamia uanzishwaji wa shule tano za msingi – Itende, Ndala, Igembe, Shiwinga na Mbalizi. Aliwateuwa walimu wafuatao ili kufundisha katika shule hizo, nao ni: John Mwaikokesya, Jason Kabunda, Angolile Mwangomo, Jotham Mwakajila na Saimon Mwanjoka. Makusudi ya shule hizo lilikuwa ni kufundisha elimu ya kawaida ya shuleni na elimu ya Kikristo. Wanafunzi walifundishwa mbinu za ushuhudiaji na kuwaleta watu kwa Yesu.

Chuo kiliendelea kukua kutoka kusajili wanafunzi 6 kwa mwaka kilipoanzishwa hadi wanafunzi 211 kwa mwaka ilipofika mwaka 2018. Tangu Chuo kuanzishwa, zaidi ya wanafunzi 3592 wameshahitimu. Wanafunzi hao walitoka sehemu mbali mbali za nchi ya Tanzania na nchi za jirani kama Rwanda, Burundi na DRC Congo. Majengo zaidi yamejengwa ili kukidhi hitaji la ongezeko la wanafunzi, walimu na wafanyakazi wa Chuo. Mengi ya majengo hayo yalijengwa na Wamishenari kwa nyakati tofauti katika historia ya Chuo. Wamishenari wanaokumbukwa ni pamoja na James Farrer, Delmer Kingsrighter, Bailey Rogers na John Ford. Baadaye bweni kubwa la ghorofa, jengo la ibada, ukumbi wa chakula na madarasa mawili yalijengwa kwa ufadhili wa Mchungaji Randy Hurst ambaye ni mtoto wa Mmishenari Wesley Hurst. Mmishenari Wesley Hurst alimaliza huduma yake hapa Tanzania mwaka 1960, kisha akaondoka akiwa ameacha kazi ya kuendeleza elimu kwa Wamishenari waliompokea.

Orodha ya Wakuu wa Chuo walioongoza chuo cha SBC

 1. Mmishenari W. Hurst (Mwanzilishi)1954 - 1960
 2. Mmishenari Norman Corre1960 - 1961
 3. Mmishenari Bellmore1961
 4. Mmishenari Marlin W. Peterson 1964 - 1967
 5. Mmishenari Jimmy Beggs 1967 - 1969
 6. Mmishenari Allen Webster 1969
 7. Mmishenari Jimmy Beggs 1970 - 1973
 8. Rev. John Mwaikokesya 1973 - 1974
 9. Mmishenari Don Ulman 1974 - 1975
 10. Mchungaji Mathias Ng’andu 1975 - 1975
 11. Mchungaji Nicodemus Mwaisabila 1975 - 1977
 12. Mchungaji Asangalwisye Kandukungonde 1977 - 1978
 13. Mchungaji Nicodemus Mwaisabila 1978 - 1985
 14. Mmishenari Bailey Rogers1985 - 1986
 1. Mchungaji Absalom Mwakyusa1986 - 1988
 2. Mchungaji Unandi Mwakafwila1988
 3. Mchungaji Edward Kinyanjui 1988 - 1990
 4. Mmishenari John Ford 1991 - 1992
 5. Mchungaji Haggai Mlumbe 1992 1993
 6. Mmishenari John Ford 1993 - 1994
 7. Mchungaji Yusufu Mbelwa 1994 - 1997
 8. Mchungaji Peter Nditi 1997 - 1998
 9. Mchungaji Samuel Mollel 1999 - 2002
 10. Mchungaji Peter Nditi 2002 - 2006
 11. Mchungaji Ronald Swai 2006 - 2007
 12. Mchungaji Jonas Mkoba 2007 - 2009
 13. Mchungaji George James 2009 - 2018
 14. Mchungaji Charles Kingu 2018 - Sasa